Wanahabari nchini Mexico, wakiwa wamevalia vifaa kinga kutokana na janga la COVID-19, wakifuatilia maandamano ya wafanyakazi wa huduma za usimamizi katika Hospitali ya Balbuena, Jiji la Mexico mnamo Aprili 16, 2020. (AFP/Pedro Pardo)

Ushauri wa Kiusalama wa CPJ: Kuripoti kuhusu janga la virusi vya corona

Imebadilishwa mara ya mwisho Agosti 14, 2020

Shirika la Afya Duniani (WHO) liliutangaza mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya COVID-19 (maarufu pia kama virusi vipya vya corona) kuwa ulioenea kote duniani, yaani pandemic mnamo Machi 11, 2020.

Wanahabari kote duniani wanatekeleza jukumu muhimu katika kuufahamisha umma kuhusu virusi hivi na juhudi za serikali za kukabiliana na virusi hivyo. Hii ni licha ya majaribio ya serikali katika mataifa kadha kudhibiti uhuru wa kuripoti na kupata habari, kama ilivyonakiliwa na CPJ. Wanahabari wanakabiliwa na shinikizo kubwa na mara kwa mara wanakuwa hatarini ya kuambukizwa kupitia kusafiri, kufanya mahojiano, na pia katika maeneo ambayo wanafanyia kazi, kwa mujibu wa mahojiano ya CPJ na wanahabari. Wanahabari wamezuiwa kutoa habari, kuzuiliwa, kushambuliwa kimwili na mtandaoni, na kupoteza mapato kutokana na COVID-19, kama ilivyoangaziwa katika ripoti za hivi karibuni za CPJ.

Hali inavyoendelea kubadilika na taarifa mpya kutokea, ushauri wa karibuni zaidi wa kiafya na taarifa zinazochipuka vitachapishwa na mamlaka husika. Ili kufahamu matukio ya karibuni zaidi, wanahabari wanaoripoti kuhusu mlipuko huu wanafaa kufuatilia taarifa kutoka kwa WHO na za mamlaka za afya nchini mwao.

Ili kupata taarifa na maelezo ya karibuni zaidi kuhusu mlipuko huu, Kituo cha Habari Kuhusu Coronavirus cha Chuo Kikuu cha John Hopkins ni chanzo salama na cha kutegemewa.

KUJIWEKA SALAMA UKIWA KAZINI KURIPOTI

Marufuku dhidi ya usafiri wa kimataifa bado zipo na zinabadilika mara kwa mara. Kazi yoyote ya kuripoti, inaweza kubadilika kukiwa na ilani ya muda mfupi au bila notisi yoyote kutokana na hali na mazingira kubadilika kwa kasi kote duniani.

Wanahabari wanaopanga kuripoti kuhusu janga la COVID-19 wanafaa kuzingatia ushauri ufuatao kuhusu usalama wao:

Kabla ya kwenda kuripoti

 • Ili kupunguza hatari ya kuambukizwa, na inapowezekana, mahojiano yanafaa kuendelea kufanywa kwa njia ya simu au kupitia mtandao badala ya kukutana na anayehojiwa
 • Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) cha Marekani, wazee na watu wenye matatizo mengine ya kiafya kama vile kisukari na tatizo la unene wamo kwenye hatari kubwa. Iwapo umo kwenye makundi hayo, unafaa kujiepusha kushiriki katika kazi ya kwenda kuripoti kuhusu virusi hivi ambayo itakukutanisha na umma. Wafanyakazi wajawazito wanafaa pia kutohusishwa.
 • Wakati wa kuwachagua watu wa kuripoti kuhusu janga la COVID-19, wasimamizi wanafaa kutilia maanani kuwa kumekuwepo visa vya mashambulio ya ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wa baadhi ya asili, kama ilivyoangaziwa na NHK World.
 • Baadhi ya mataifa ambayo awali yaliyoondoa hatua zilizowekwa za kuwazuia watu kutoka nje na kutangamana hivi yamerudi kuzitekeleza tena, kama ilivyoripotiwa na Forbes. Kwa hivyo, unafaa kujadili ni mipango gani ambayo wasimamizi wako wanayo ya kukusaidia iwapo utaugua ukiwa kazini kuripoti, na uzingatie pia uwezekano wa kujitenga na/au kujipata kwenye eneo ambalo watu wamezuiwa kutoka/kuwekwa kwenye karantini kwa kipindi kirefu

Afya ya kiakili

 • Wanahabari wote, hata wale wenye uzoefu sana, wanaweza kutatizika kiakili wanaporipoti kuhusu mlipuko wa COVID-19, kwa mujibu wa Taasisi ya Reuters katika Chuo Kikuu cha Oxford. Wasimamizi wanafaa kuwafuatilia wanahabari wao mara kwa mara kujua hali yao, na kutoa ushauri na usaidizi iwapo na wakati unapohitajika
 • Ndugu na jamaa zako wanaweza kuwa na wasiwasi na hofu wakisikia kuwa unapanga kuripoti kuhusu mlipuko wa COVID-19. Zungumza nao kuhusu hatari zilizopo na wasiwasi wao. Ikiwezekana, panga mazungumzo kati yao na washauri wa afya wa shirika lako.
 • Wanahabari wameiambia CPJ kwamba wanaporipoti kuhusu COVID-19, hata jamaa zao na marafiki wameuliza kuhusu hatari zilizopo, na mara nyingi kueleza wasiwasi wao. Hili linaweza kuvunja moyo
 • Fikiria athari za kiakili zinazoweza kutokana na kuripoti kutoka eneo lililoathiriwa na COVID-19, hasa iwapo unaripoti kutoka kituo cha afya au kituo cha kuwatenga watu, au eneo la karantini. Maelezo muhimu kwa wanahabari wanaofanya kazi katika mazingira hatari na ya kutia kiwewe yanaweza kupatikana kupitia kituo cha  DART Center cha Uanahabari na Kiwewe. Tembelea ukurasa wa Dharura wa CPJ kwa rasilimali zaidi kutoka vyanzo vya nje kuhusu kujiweka salama, zikiwemo ushauri wa kujiweka salama kiakili kama mwanahabari anayeripoti kuhusu COVID-19.

Kujikinga dhidi ya Maambukizi & Kuwaambukiza wengine

Mataifa mengi kwa sasa yanatekeleza ushauri wa watu kutokaribiana, ingawa umbali unaohitajika ni tofauti kutoka taifa moja hadi jingine,kwa mujibu wa Reuters. Iwapo unaenda kuripoti katika eneo lenye watoaji huduma za dharura au unatembelea maeneo yenye hatari kubwa kwa mfano haya yaliyoorodheshwa hapa chini, uliza awali kuhusu hatua za usafi na usalama ambazo zinatekelezwa humo. Ukiwa na shaka zozote, usizuru:

 • Kituo chochote cha afya
 • Kituo au makao ya kuwatunza wazee
 • Nyumbani kwa mtu anayeugua na/au mzee, mtu aliye na matatizo ya kiafya, au mja mzito
 • Kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa ambapo hatari ya kuambukizwa inaaminika juu, kwa mfano kiwanda cha nyama
 • Mochari au chumba cha kuhifadhia maiti, tanuu ya kuchomea maiti, au panapofanyiwa ibada ya wafu
 • Karantini, eneo walimotengwa watu, au eneo ambalo watu hawaruhusiwi kuingia au kutoka
 • Maeneo yanayoishi watu wengi mijini (kwa mfano mtaa wa mabanda)
 • Kambi ya wakimbizi
 • Jela au kituo cha kuwazuilia watu ambapo kumeripotiwa visa vya COVID-19

Ili kujikinga na maambukizi, unashauriwa kuchukua hatua zifuatazo:

 • Kaa umbali uliopendekezwa kati yako na wengine, ambao ni tofauti kwa kutegemea ushauri wa kiafya kutoka mamlaka hadi nyingine. Unafaa kuwa makini zaidi hasa ukiwa karibu na watu walio na dalili za ugonjwa wa kupumua, kwa mfano kukohoa na kupiga chafya na/au unapowahoji wazee, wale walio na matatizo mengine ya kiafya, mtu yeyote aliyemkaribia mgonjwa anayeonyesha dalili, wahudumu wa afya wanaowahudumia wagonjwa wa COVID_19, na watu wanaofanya kazi kwenye eneo lolote la hatari kubwa.
 • Kila wakati jaribu kuwahoji watu katika maeneo yaliyo wazi. Iwapo utahitajika kufanya mahojiano ndani ya nyumba, chagua pahala ambapo pana mtiririko mzuri wa hewa (mfano karibu na madirisha yaliyo wazi) na ujiepushe na vyumba vidogo au maeneo yasiyo na nafasi kubwa
 • Usimsalimie mtu yeyote kwa mikono, kukumbatiana na/au kupigana busu na mtu yeyote
 • Jaribu kusimama ukiwa umegeuka kidogo badala ya kumwangalia unayemhoji ana kwa ana, na ukumbuke kila wakati kukaa umbali wa uliopendekezwa.
 • Osha mikono yako vyema mara kwa mara kwa maji moto na sabuni, kwa muda wa angalau sekunde 20. Hakikisha mikono yako imekaushwa kwa njia nzuri. Mwongozo muhimu kuhusu jinsi ya kuosha na kukausha mikono yako vyema upapatikana katika tovuti ya WHO
 • Iwapo hauna maji moto na sabuni, tumia vitakasa mikono au vitambaa vyenye kemikali ya kuua bakteria, lakini hakikisha kwamba baadaye unaosha mikono kwa maji moto na sabuni ukipata fursa hiyo (CDC inapendekeza watu watumie vitakasa mikono vyenye kilevi cha angalau 60% ethanol au 70% isopropanol. Usitumie matumizi ya vitakasa mkono kama mbadala wa kuosha mikono mara kwa mara
 • Kumbuka kufunika mdomo wako na pua unapokohoa au kupiga chafya. Unafaa kukohoa au kupiga chafya ukitumia karatasi ya shashi yaani tissue na uhakikishe unaitupa pahala salama mara moja, na kisha ukumbuke kuosha mikono vyema baadaye
 • Jiepushe kujigusa uso, pua, mdomo, masikio na kadhalika kama ilivyoangaziwa na BBC
 • Jiepushe kunywa/kula kwa kutumia vikombe, sahani, uma au vijiko ambavyo huenda vimetumiwa au kuwa karibu na watu wengine
 • Nywele zote zinafaa kufunikwa vyema. Iwapo una nywele ndefu, zinafaa kufungwa na kufunikwa vyema.
 • Vua vito vyote na mapambo pamoja na saa kabla ya kwenda kazini kuripoti, ukikumbuka kwamba virusi hivi vinaweza kusalia vikiwa hai kwenye vitu vya aina nyingi kwa muda tofauti tofauti
 • Iwapo huwa unavalia miwani, isafishe kwa makini mara kwa mara kwa kutumia maji moto na sabuni
 • Usivalie lensi zinazoambatanishwa na mboni za macho ukiwa kazini kuripoti, ikiwezekana, kutokana na uwezekano wako wa kuyagusa macho yako na kuongeza uwezekano wako kuambukizwa
 • Fikiria ni nguo gani utavalia, kwa kuzingatia kwamba baadhi ya vitambaa vitaweza kupanguswa kwa wepesi kuliko vingine. Mavazi yote yanafaa kuvuliwa kwa umakinifu na kuoshwa kwa maji moto na kwa kutumia dawa kali au sabuni ya kusafishia baada ya kutoka kuripoti
 • Ikiwezekana, jaribu kujiepusha kutumia pesa taslimu ukiwa kazini kuripoti, na uhakikishe unasafisha au kutakasa kadi zako za benki, kipochi, na/au mkoba wako mara kwa mara. Jiepushe kuweka mikono yako kwenye mifuko yako kadiri inavyowezekana.
 • Fikiria kuhusu njia yako ya kusafiri kwenda na kurudi kutoka eneo unaloenda kuripoti. Jiepushe na usafiri wa umma nyakati za watu wengi kusafiri na pia hakikisha unatakasa mikono yako kwa kutumia vitakasa mikono unaposhuka.
 • Iwapo unasafiri kwa kutumia gari lako au gari la kampuni, fahamu kwamba mtu yeyote aliyeambukizwa ndani ya gari hilo anaweza kuwaambukiza wengine ndani ya gari hilo, kama ilivyoangaziwa majuzi na BBC nchini India. Hakikisha mkiwa safarini madirisha ya gari yako wazi kuwezesha mtiririko mzuri wa hewa ndani ya gari, na ikiwezekana mvalie vitambaa vya usoni au barakoa mkiwa ndani ya gari
 • Pumzika mara kwa mara na uzingatie viwango vya nguvu/sukari mwilini mwako, ukikumbuka kwamba watu waliochoka wana uwezekano mkubwa sana wa kufanya makosa katika kudumisha usafi. Pia, zingatia kwamba watu wanaweza kuhitajika kusafiri mwendo mrefu kabla na baada ya kazi
 • Hakikisha unanawa mikono vyema kila wakati kwa kutumia maji moto na sabuni kabla, wakati, na baada ya kuondoka eneo lililoathiriwa
 • Iwapo utaanza kupata dalili za kuugua, hasa homa au kushindwa kupumua, panga jinsi ya kupata huduma ya matibabu. Taasisi nyingi za afya za serikali zinapendekeza ujiweke kwenye karantini kuzuia kuwaambukiza wengine. Iwapo umo katika eneo lenye visa vingi vya maambukizi, unaweza kuwa kwenye hatari ya kukutana na wagonjwa walioambukizwa COVID-19 katika maeneo yenye watu wengi, hivyo kuongeza uwezekano wa kuambukizwa
 • Iwapo utakula nyama na mayai, hakikisha vimepikwa vyema

Usalama wa Vifaa

Kuna hatari ya kusambazwa kwa COVID-19 kupitia vifaa na mitambo iliyoambukizwa. Vifaa vyote vinafaa kuoshwa vyema na kutakaswa wakati wote:

 • Tumia maikrofoni zinazoweza kunasa sauti ukiwa mbali, maarufu kama ‘fishpole’ iwapo inawezekana. Maikrofoni ndogo za kuvaliwa na anayehojiwa zinafaa kutumiwa tu katika mazingira yaliyodhibitiwa pekee, na watu wafuate ushauri wa usalama wa kiafya kikamilifu.
 • Vifuniko vya maikrofoni vinafaa kutakaswa na kuoshwa vyema kwa sabuni na maji moto baada ya kurejea kutoka kazi yoyote ya kuripoti. Tafuta ushauri/mafunzo kuhusu jinsi ya kuvitoa vifuniko kwa njia salama kutoka kwa maikrofoni kuzuia kusambazwa zaidi kwa virusi Jaribu kutotumia vifuniko ‘vya manyoya’ ikiwezekana kwani ni vigumu kuviosha na kuvitakasa
 • Tumia vidude vya kusikilizia vya gharama ya chini ikiwezekana na vitupwe baada ya kutumiwa, hasa kwa wageni. Pangusa na kutakasa vifaa vyote vya kusikilizia kabla na baada ya kutumiwa
 • Tumia lensi zinazoweza kunasa picha au video kutoka mbali ili kukusaidia kukaa umbali ufaao ukiwa kazini
 • Ikiwezekana, tumia vifaa vinavyopeperusha mawasiliano au data kupitia hewani badala ya zinazotumia nyaya
 • Fikiria jinsi ya kuhifadhi vifaa vyako ukiwa kazini kuripoti. Usiache kitu chochote kikae kiholela na hakikisha umeweka kila kifaa kwenye sanduku au mkoba wake na kufungia vyema (kwa mfano, tumia mikoba migumu ya kusafiria kwenye ndege ambayo huwa rahisi kupangusa na kuiweka ikiwa safi)
 • Ikiwezekana, tumia vifungashio vya plastiki au kitu kingine cha kufunika au kukinga vifaa vyako unapovitumia. Hii itapunguza sehemu za vifaa vyako ambazo zinaweza kuambukizwa, na itakuwa rahisi kusafisha na kutakasa baadaye
 • Beba betri za ziada zilizojaa chaji na uepuke kuweka chaji ukiwa eneo uliloenda kuripoti, kwani vifaa vya kuchajia vitakuwa ni vitu vya ziada vinavyoweza kuambukizwa
 • Kila wakati, takasa vifaa vyako kwa kemikali za kuua bakteria haraka kama vile Meliseptol, na baadaye uhakikishe pia unavisafisha vifaa vyote zikiwemo simu za mkononi, tablet, vihifadhia data yaani hard drives, kamera, vitambulisho na kamba za kufungia vitambulisho
 • Hakikisha vifaa vyote vimetakaswa tena unapovirejesha afisini mwenu, na kuhakikisha kwamba wanaovihifadhi wanafahamishwa mapema na kwamba wamefunzwa jinsi ya kuvitakasa vifaa hivyo. Hakikisha kwamba vifaa haviwekwi tu kiholela afisini bila kuhakikisha vimekabidhiwa mtu anayefaa kuvisafisha na kuvitakasa
 • Iwapo mtatumia gari wakati wa kuripoti, hakikisha kwamba limesafishwa vyema kwa undani na watu waliofunzwa vyema baada ya kurejea kutoka kazi ya kuripoti, ikiwezekana na mtu aliyepewa mafunzo vyema. Uangalizi zaidi unafaa kuwa kwenye vipete vya kufungulia milango, kifaa cha kubadilishia gia, handibreki, usukani, vioo vya kuangalia nyuma, misamilo yaani head rests, mikanda ya usalama, dashibodi, na vitufe au vidude vya kupandishia na kushushia vioo vya gari

Kuvisafisha Vifaa vya Kielektroniki

Hapa chini tumeorodhesha baadhi ya mambo unayoshauriwa kuzingatia kwa kawaida wakati wa kuvisafisha vifaa vyako vya kielektroniki. Hakikisha kila wakati kwamba umesoma mwongozo wa mtengenezaji wa kifaa kabla ya kujaribu njia yoyote ya kukisafisha.

 • Kila wakati toa/chomoa kifaa kutoka kwenye nguvu za umeme, vifaa vingine, na nyaya
 • Usiweke vitu viowevu au majimaji karibu na kifaa chako, na usitumie vipulizaji vya erosoli, kemikali za kupausha au kuondoa rangi na kufanya kitu kuwa cheupe, na vitu vinavyochubua au kukwaruza – kwani sana sana hivi vyote vitaharibu kifaa chako
 • Usipulizie kitu chochote moja kwa moja kuelekea kwenye kifaa chako
 • Tumia kitambaa kisichokwaruza, laini na kisichokuwa na nyuzi za pamba
 • Kifanye kitambaa chako kiwe na unyevu kidogo, lakini KISILOWE. Mwagia au kupaka sabuni kwenye kitambaa na uisugue kwa mkono wako kwenye kitambaa
 • Pangusa kifaa chako vyema mara kadha kwa kutumia kitambaa hicho
 • Usikubali unyevu wowote ufikie matundu au mashimo yoyote (kwa mfano matundu ya kuwekea chaji, vitundu vya kuingizia vifaa vya kusikilizia, na kibodi)
 • Kausha kifaa chako kwa kukipangusa kwa kutumia kitambaa safi kilichokauka na kilicho
 • Baadhi ya watengenezaji wa vifaa hupendekeza matumizi ya vitaa vya kupangusia vyenye kilevi aina ya isopropyl kwa kiwango cha 70% kusafisha maeneo ya vifaa yasiyoingiza unyevu
 • Iwapo unatakasa vifaa vyako, ni vyema kutafuta ushauri wa mtengenezaji wa vifaa hivyo kwanza, kwani vitakasa vinaweza kuharibu kifaa chako.

Unaweza kupata ushauri zaidi na wa kina kupitia taarifa hii.

Vifaa vya Kukinga Mwili (PPE)

Kuvalia na kuvua vifaakinga au PPE za kimatibabu (kwa mfano glavu, barakoa au mask, aproni za kujikinga/ovaroli/ vazi maalum la kukinga mwili dhidi ya maambukizi linaloufunika mwili wote, na vifunikia viatu na kadhalika) ni jambo linalohitaji mtu kufuata ushauri wa kiusalama kwa umakinifu. Tafadhali bofya hapa kusoma ushauri kutoka kwa CDC. Unafaa kuwa makini zaidi unapovua vifaakinga, kwani wakati huo ndio hatari ya kuambukiza ilipo juu zaidi, kwa hivyo usilegeze hatua hizi. Iwapo una shaka, tafuta ushauri wa wataalamu na upokee mafunzo kabla ya kwenda kazi yoyote ile kuripoti

Fahamu kuwa katika mataifa mengi bado kuna uhaba wa vifaakinga vya kimatibabu na hivyo basi ni vigumu kupata vifaa hivyo, kwa hivyo kuvitumia kunaweza kuchangia uhaba zaidi.

 • Hakikisha PPE yoyote unayoivaa inakutoshea vyema. Vifaa kinga visivyokutoshea vyema vinaweza kuraruka au kupasuka na/au kukuzuia kutembea au kufanya shughuli nyingine (iwapo vitabana sana), na pia vinaweza kukwamilia vyenye vitu kama vile kipete cha kufunga au kufungua mlango na pia kuraruka (iwapo ni kubwa zaidi haijakutoshea vyema au inapwaya)
 • Kila wakati hakikisha unatumia vifaakinga vya kimatibabu vya kampuni zinazotambulika, na uzingatie sana viwango vya chini zaidi vya kiusalama vinavyohitajika. Fahamu kuwa zipo zilizo na kasoro, kama ilivyoangaziwa na The New York Times, na kunazo hata ghushi, kama ilivyoangaziwa na mtandao wa Securing Industry. Unaweza kupata baadhi ya nembo zinazoongoza na zinazotambulika sana hapa.
 • Tumia glavu za kujikinga iwapo unafanya kazi katika au unatembelea kituo kilichoambukizwa kwa mfano kituo cha kuwatibu wagonjwa. Fahamu kuwa glavu za nitrile zinatoa kinga ya juu zaidi kuliko za latex. Kuvalia glavu mbili kila mkono kunaongeza kinga
 • Iwapo unaripoti kutoka katika eneo la hatari kubwa kama vile kituo cha kuwatibu wagonjwa, kuna uwezekano mkubwa kwamba utahitaji PPE za kimatibabu kama vile vazi maalum la kukinga mwili dhidi ya maambukizi linaloufunika mwili wote na barakoa za ziada
 • Iwapo unatumia bwelasuti au vazi linaloufunika mwili wote, hakikisha umekwenda haja msalani kabla ya kuivalia PPE hiyo
 • Kwa kutegemea kazi yako ya kuripoti, unaweza ukahitaji viatu vya kuvaliwa kwa muda au buti zisizoingiza maji za kuvaliwa juu ya viatu vya kawaida, na vyote ni lazima vipanguswe/kuoshwa baada yako kuondoka eneo lililoathiriwa na virusi. Iwapo unatumia buti zisizoingiza maji, zinafaa kutupwa kwa njia salama kabla ya kuondoka eneo hilo
 • Inashauriwa kwamba PPE zote za kimatibabu zivaliwe chini ya uangalizi wa mtaalamu aliyepokea mafunzo, kwa kuzingatia kwamba huu unaweza kuwa wakati wa kukumbana na virusi. Video hii ya kuvalia na kuvua vifaa kinga kutoka kwa CDC inaweza kufaa, ingawa haifai kutumiwa kama mbadala wa kupewa mafunzo/kuwa na mwangalizi
 • Usitumie PPE za kutumiwa mara moja zaidi ya mara moja kwa mfano glavu, mavazi ya kukinga mwili, aproni, au vifunikia viatu. Vifaa vyote ambavyo vinahitajika kutumiwa tena ni lazima viafishwe na kutakaswa vyema. Hakikisha PPE zote zilizovaliwa zimetupwa kwa njia ifaayo KABLA ya kuondoka eneo lililoathiriwa

Barakoa au mask

Kutumia mask au barakoa ipasavyo ni muhimu sana hasa kwa wanahabari ambao wanaendelea kuripoti kutoka maeneo yenye watu, jambo linalomaanisha kwamba wanaweza kuingia maeneo yaliyofungana, maeneo yenye watu wengi, na kuzungumza na umma. Mnamo Julai 9,2020, WHO ilitoa ushauri mpya na kueleza kuwa kuna uwezekano COVID-19 ni ugonjwa unaoweza kusambaa kupitia hewa katika maeneo maalum. Maeneo hayo ni kama (lakini si hayo pekee) maeneo yaliyofungana yasiyo na mtiririko mzuri wa hewa na pia maeneo yenye watu wengi. Unafaa kufahamu kwamba kiwango virusi hewani katika maeneo kama hayo kinaweza kuwa cha juu kuliko kawaida, na hivyo kuongeza hatari ya kuambukizwa.

Mataifa mengi sasa yanahitaji na/au yanawashauri wananchi kuvalia vitambaa vya kujifunika usoni na/au barakoa maeneo ya umma, kama ilivyoripotiwa na Al-Jazeera. CDC inashauri watu kuvalia vifunikia nyuso vyenye matabaka matatu ya vitambaa – lakini si barakoa za kimatibabu, ambazo bado kuna uhaba – kufunikia pua na mdomo mtu akiwa maeneo yenye watu. WHO inashauri kuwa mtu yeyote mwenye umri wa miaka 60 na zaidi, pamoja na wale wenye matatizo mengine ya kiafya, wavalie barakoa za kawaida za kimatibabu wakiwa nje maeneo yenye watu na hawawezi kukaa mbali na wengine. Wanashauri kuwa watu wengine wote wavalie barakoa za vitambaa vya kawaida zenye matabaka matatu.

Zisipotumiwa vyema, kuna wasiwasi kwamba barakoa zinaweza kuwa chanzo cha maambukizi. Utafiti wa karibuni wa Lancet unaonyesha kulikuwa na masalio ya virusi kwenye barakoa ya kimatibabu kufikia siku saba baada ya kuwa kwenye eneo lenye virusi. Kwa kuzingatia utafiti huu, kuvua au kutumia tena barakoa, au kuugusa uso wako unapokuwa umevalia mask kunaweza kukuweka hatarini ya kuambukizwa.

Iwapo utavalia barakoa, unafaa kufuata ushauri ufuatao:

 • Ikiwa itahitajika, barakoa aina ya N95 (au FFP2/FFP3) ndiyo inayopendekezwa badala ya barakoa ya kawaida ya wakati wa upasuaji.
 • Hakikisha kwamba barakoa hiyo inatoshea vyema kutoka kwenye juu ya pua hadi kwenye kidevu, na kupunguza mianya. Hakikisha kwamba umenyoa ndevu na masharafa na kuhakikisha barakoa inaunata na kuufunika vyema uso wako. Fahamu kwamba kuwa na ndevu zilizoota au masharafa kutazuia barakoa yako kuunata uso vyema.
 • Ni muhimu sana kufuata ushauri wa kiusalama kikamilifu unapoitumia barakoa. Jiepushe kuigusa barakoa upande wa nje, na uivue tu kwa kuvuta kamba zake. Kadhalika, epuka kujaribu kuibadilisha badilisha au kujaribu kuiweka sawa mask yako baada ya kuivalia ila tu iwapo itabidi. Osha mikono yako papo hapo iwapo utaigusa mask yako.
 • Kutumia barakoa zaidi ya mara moja ni hatari kubwa. Hakikisha unaitupa mask yako mara moja baada ya kuitumia kwa kuiweka ndani ya mfuko unaofungika.
 • Osha mikono kwa sabuni na maji moto, au kwa kutumia kemikali ya kutakasa mikono iliyo na kilevi (zaidi ya 60% kwa ethanol au 70% kwa isopropanol) baada ya kuvua barakoa
 • Badilisha mask kwa nyingine mpya iliyokauka baada ya ile unayotumia kulowa au kuwa na majimaji
 • Kumbuka kwamba matumizi ya barakoa ni sehemu moja tu ya kujikinga. Jiepushe kugusa uso wako, pua na macho na uhakikishe unaosha mikono yako mara kwa mara kwa maji moto na sabuni.
 • Fahamu kwamba barakoa zinaweza kuadimika na/au bei yake kupanda pakubwa, kwa kutegemea eneo

Usalama wa Kidijitali

 • Fahamu kwamba wanahabari wanaweza kukabiliwa na viwango vya juu vya uadui kutokana na wanavyoripoti kuhusu mlipuko wa COVID-19. Soma ushauri wa CPJ kuhusu njia za kujikinga dhidi ya mashambulio mtandaoni
 • Serikali na kampuni za teknolojia zinazidisha kutumia upelelezi wa kuwafuatilia na kuwachunguza watu kama njia ya kufuatilia kusambaa kwa COVID-19. Hii ni pamoja na  NSO Group, ambayo imeunda Pegasus, ambayo ni programu ya kijasusi ambayo imetumiwa kuwaandama wanahabari, kwa mujibu wa Citizen Lab. Makundi ya kutetea haki za kiraia yamekuwa yakieleza wasiwasi wao kuhusu jinsi teknolojia hizi zitakavyotumika kuwafuatilia watu baada ya mzozo huu wa kiafya kumalizika. Shirika la Transparency International limekuwa likifuatilia matukio haya kwenye tovuti yake
 • Simama na kufikiria kabla ya kubofya kwenye kiunganisho au link mtandaoni au kupakua nyaraka zinazodaiwa kuwa na maelezo kuhusu COVID-19. Wahalifu wanatumia mzozo wa sasa wa afya na wasiwasi uliopo kuwalenga watu binafsi kwa barua pepe za kutumiwa kama chambo yaani phishing emails ambazo zinaweza kusababisha programu hasidi au zenye madhara kuwekwa kwenye vifaa vyako vya kielektroniki, kwa mujibu wa Electronic Frontier Foundation
 • Kuwa makini sana unapobofya kwenye viunganisho au link zozote kuhusu COVID-19 kwenye mitandao ya kijamii au app za kuwasiliana kwa kutumia ujumbe, baadhi ambazo huenda zikakuelekeza kwenye tovuti zinazoweza kuambukiza kifaa chako programu hasidi au zenye madhara
 • Jihadhari sana na app zinazowalenga watu kwa kutumia programu za kuteka kompyuta au simu na kudai malipo, kwa mfano COVID-19 Tracker
 • Ramani zilizo na maelezo na habari za karibuni zaidi kuhusu COVID-19 kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika, kama vile WHO, zimeripotiwa kuwa na programu hasidi zinazoweza kuiba nywila au passwords
 • Kuwa makini kuhusu taarifa za uzushi ambazo zinaweza kuwa zinaenezwa na vyombo vya serikali, kama ilivyoripotiwa na The Guardian, pamoja na taarifa za uzushi za kawaida, jambo ambalo WHO imetahadharisha sana kuhusu na BBC imeangazia. Mwongozo wa kutambua habari hizi za uzushi unapatikana katika mtandao wa WHO
 • Kuwa makini kuhusu habari kuhusu COVID-19 zinazoenezwa kupitia app za kutuma ujumbe, ambazo zinaweza kuwa za uzushi au za kupotosha
 • Fahamu kuwa taarifa kuhusu COVID-19 kwenye Facebook siku hizi zinatathminiwa na teknolojia ya kufikiria ya kompyuta (AI) badala ya watu halisi, jambo ambalo limesababisha taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huu kufutwa kimakosa
 • Soma kuhusu kuwasiliana na kuandaa mikutano kupitia mtandao na masuala ya faragha ili kufahamu huduma hizi zinafanya nini na data yako, wanaweza kupata data gani kutoka kwako, na ni salama kiasi gani. Fahamu kuwa huku watu wanaofanyia kazi manyumbani mwao ikiongezeka, huduma hizi zimelengwa na wadukuzi
 • Tahadhari kuhusu hatari zinazotokana na kuripoti kuhusu na/au kutoka mataifa yenye uongozi wa kiimla, ambayo kuna uwezekano yatakuwa yanafuatilia kwa karibu ripoti kuhusu mlipuko wa COVID-19. Baadhi ya serikali zinaweza kujaribu kuficha ukweli kuhusu kuenea kwa mlipuko na/au kuzuia vyombo vya habari kuripoti ukweli, kama ilivyoangaziwa na CPJ

Uhalifu & Usalama wako Ukiwa Kazini Kuripoti

Wanahabari na wafanyakazi katika mashirika ya habari wanafaa kufahamu kuwa kuna ongezeko la hisia dhidi ya waandishi wa habari na kuongezeka kwa chuki dhidi yao, ikiwa ni pamoja na matusi au hata kushambuliwa wakiwa kazini kuripoti, kama ilivyoshuhudiwa majuzi Marekani, – kwa mujibu wa US Freedom Tracker – Ujerumani, Uingereza, India na Somalia.

Hali ya uchumi duniani inatarajiwa kuendelea kudorora, na watu kupoteza nafasi zao za kazi na watu karibu nusu bilioni wamo hatarini ya kutumbukia kwenye umaskini, kwa mujibu wa Oxfam. Uwezekano wa kuongezeka kwa visa vya uhalifu ni mkubwa, hasa uhalifu wa kimtandaoni, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Cambridge.

 • Iwapo unaweza kusafiri kwenda kuripoti nje ya nchi yako (soma hapa chini), tafiti kuhusu hali ya karibuni zaidi ya kiusalama unakoenda. Ingawa fujo na ghasia zimepungua, kuwekuwepo na visa vya ghasia na maandamano maeneo mbalimbali duniani tangu mwisho wa Februari. Fahamu kuwa ghasia na fujo zinaweza kuzuka tena iwapo hatua zilizochukuliwa kuwazuia watu zitatekelezwa tena kutokana na wimbi la pili la maambukizi.
 • Maeneo mengi ya miji kwa sasa hayana watu na shughuli nyingi kama kawaida na polisi wanazidiwa na kazi. Kuna hatari kwamba wahalifu wanaweza kutumia fursa hii kutekeleza uhalifu. Baadhi ya wanahabari wameripoti visa vya kurushiwa maneno na kulengwa na wahalifu, pamoja na kushambuliwa, na kwa hivyo usipuuze usalama wako
 • Kuwa makini zaidi iwapo unaripoti kutoka maeneo ya mashambani. Watu wanaweza kushuku na/au kuwa na hasira dhidi ya “watu kutoka nje” kwa hofu kuwa huenda wakawapelekea COVID-19
 • Fahamu kuwa kuna uwezekano wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi wakitekeleza maagizo ya watu kutotoka nje kutokana na COVID-19, kwa vitendo kama vile kuwapiga watu na kutumia risasi halisi, vitoa machozi na risasi za mipira
 • Iwapo unaripoti kutoka gerezani au kituo cha kuwazuilia watu, kama mwanahabari unafaa kufahamu hatari inayoweza kutokana na wafungwa au mahabusu iwapo wataandamana na/au kuzua fujo kuhusiana na mlipuko wa COVID-19, kama ilivyoshuhudiwa awali Sierra Leone, Italia, Nigeria, Colombia, na India
 • Fahamu kuwa kuna uwezekano wa visa vya uhalifu kuongezeka, ukitilia maanani kwamba mataifa kama vile Iraq, Marekani, Ireland, Indonesia, Ethiopia, Palestina, Somaliland, na Iran yamewaachia huru wafungwa ili kupunguza msongamano wa wafungwa wakati wa mlipuko wa COVID-19.
 • Kuwa macho kuhusu uwezekano wa visa vya uporaji na wizi kutokea, hasa iwapo hatua za kuwazuia watu zitaanza kutekelezwa tena na/au viwango vya ukosefu wa ajira kuongezeka
 • Wanahabari katika mataifa yenye serikali za kiimla wanafaa kufahamu na kuzingatia hatari ya kuzuiliwa, kukamatwa na/au kufurushwa kutoka nchi husika wakiripoti kuhusu mlipuko wa COVID-19, kama ilivyoangaziwa na CPJ

Kwenda kuripoti nje ya nchi

Kutokana na marufuku na vikwazo vya usafiri vilivyotolewa na mataifa mengi duniani, inaendelea kuwa vigumu kusafiri nje ya nchi. Hata hivyo, iwapo inawezekana kwenda kuripoti nje ya nchi yako, unafaa kuzingatia yafuatayo:

 • Fahamu kuwa hatua za kuwazuia watu na/au amri ya kutoka nje zote zinaweza kuwa tofauti kutoka sehemu moja ya nchi hadi nyingine. Fahamu kuwa hatua za kuwazuia watu zinaweza kutekelezwa kukiwa na notisi ya muda mfupi au hata bila notisi.
 • Hatua za kuwaweka watu wanaorejea nchi fulani karantini zinaweza kuanza kutekelezwa au kubadilishwa kukiwa na ilani ya muda mfupi au bila ilani yoyote kwa kutegemea eneo ulilolitembelea, kama ilivyoshuhudiwa majuzi kwa watu waliokuwa wakirejea Uingereza kutoka Uhispania.
 • Vitambue vituo vyote vya matibabu vilivyo eneo unakofanya kazi. Fahamu kuwa wahudumu wa afya wanaweza kugoma au kufanya maandamano wakiwa wametoa notisi ya muda mfupi au bila notisi hata kidogo, kama ilivyotokea mataifa mbalimbali yakiwemo India, Sierra Leone, Nigeria na Ufaransa.
 • Huenda kukawa na uhaba wa PPE na/au hata ziwe hazipatikani hata kidogo. Hakikisha kwamba kila wakati unafanya utafiti mapema kabla ya kusafiri, na kujibebea za ziada ikiwa itahitajika.
 • Hakikisha umetimiza masharti yote ya chanjo na kinga za magonjwa yanayohitajika katika taifa hilo kwa wakati. Ni vyema ukapata chanjo dhidi ya mafua ili kuzuia utata kuhusu dalili za ugonjwaambazo huenda ukawa nazo
 • Angalia vyema bima yako ya usafiri, ukifahamu kwamba huenda ikawa vigumu kupata bima ya kusafiri maeneo yaliyo na COVID-19. Fahamu kuwa mataifa mengi yametoa ushauri na tahadhari za viwango tofauti dhidi ya kusafiri kuingia mataifa hayo.
 • Mara kwa mara angalia yanayojiri kuhusu hafla yoyote unayopanga kuhudhuria, kwa kuzingatia kwamba mataifa mengi yamepiga marufuku mikusanyiko ya watu kuanzia kiasi fulani.
 • Chunguza iwapo kuna/au kunapangwa marufuku za usafiri eneo unalopanga kusafiri, ukifahamu kwamba hali inaweza kubadilika kwa notisi fupi.
 • Hakikisha una mpango wa kuchukua kukitokea dharura, kwa kuzingatia kwamba miji, baadhi ya maeneo, na/au mataifa yanaweza kuwekewa marufuku ya usafiri na kuwekwa karantini kukiwa na notisi ya muda mfupi sana au bila hata ilani. Baadhi ya mashirika na waajiri wameongeza kiwango chao cha kujiandaa kuwaondoa watu wao walio katika mataifa mbalimbali duniani
 • Mataifa mengi yameendelea kufunga mipaka yake.Mipaka inayoweza ikafunguliwa inaweza pia kufungwa tena bila tahadhari, jambo ambalo unafaa kulizingatia wakati wa kuandaa mpango wako wa kuchukua hatua wakati wa dharura.
 • Usisafiri iwapo unaugua. Viwanja vingi vya kimataifa na kikanda, pamoja na vituo vingi vya usafiri, vimetekeleza masharti makali ya watu kupimwa afya yao. Wasafiri wanaweza kupimwa na/au kuwekwa karantini/kutakiwa kujitenga kwa lazima baada ya kuwasili
 • Nyenzo za kusafiri maeneo mbalimbali duniani bado ni chache sana kutokana na mashirika ya ndege kufuta safari zao kwenda/kutoka maeneo mengi.
 • Fahamu kuwa COVID-19 imesababishia mashirika ya ndege hasara kubwa kifedha, kwa mujibu wa taarifa za habari, kwa hivyo fikiria uwezekano wa kununua tiketi za ndege ambazo unaweza kurejeshewa nauli yote ukikosa kusafiri.
 • Tafakari ni vitu gani unaweza kuhitaji kuvibeba. Ingawa visa vya watu kununua kwa wingi na kuhodhi vitu mbalimbali vinaonekana kupungua, hauwezi kufutilia mbali uwezekano wa uhaba wa vitu kama vile barakoa au mask, vitakasa mikono, sabuni, vyakula vya mikebe na karatasi za shashi/chooni siku za usoni, na hilo linafaa kuzingatiwa. Fahamu kwamba migomo na/au uhaba wa wafanyakazi kutokana na maambukizi ya COVID-19 vinaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi unakoenda
 • Angalia hali ya karibuni zaidi kuhusu viza unakoenda, ukitambua kwamba mataifa mengi yamesitisha utoaji wa viza na kusimamisha viza ambazo zilikuwa tayari zimetolewa kwa usafiri
 • Chunguza iwapo taifa unakoenda linahitaji cheti cha kimatibabu cha kuthibitisha kwamba hauna COVID-19.
 • Kuwa na ratiba inayoweza kubadilishwa kwa urahisi na utenge muda wa ziada wa kupitia viwanja vya ndege maeneo mbalimbali, kwa kuzingatia vipimo vya ziada vya afya na vituo vya kupima watu joto. Vilevile katika baadhi ya vituo vya treni, bandari/gati, na vituo vya usafiri wa mabasi ya masafa mrefu
 • Jifahamishe kuhusu mabadiliko yoyote yanayotokea eneo unakoenda, na ufahamu kwamba baadhi ya mataifa yanaruhusu tu raia wa nchi za nje kuingia katika mataifa hayo kwa kutumia viwanja na vituo fulani
 • Fuatilia vyombo vya habari mara kwa mara kupata taarifa za iwapo kuna vikwazo vipya vya usafiri kutoka eneo moja la jiji hadi jingine katika nchi unayozuru

Baada ya kuripoti

 • Fuatilia hali yako ya afya mara kwa mara kubaini iwapo una dalili
 • Huenda ukalazimika kujitenga baada ya kutoka kuripoti kutoka eneo lenye hatari kubwa. Tafadhali chunguza ushauri husika wa serikali
 • Fuatilia taarifa na habari za karibuni zaidi kuhusu COVID-19, pamoja na utaratibu wowote wa karantini au kujitenga unaotekelezwa unakotoka na unakoenda
 • Kwa kutegemea kiwango cha maambukizi katika taifa ulilomo, unafaa kutafakari uwezekano wako kuweka shajara au kitabu kidogo chenye majina/nambari za simu za watu ambao unatangamana nao kwa siku 14 baada yako kurejea. Hii itasaidia katika kuwatafuta iwapo utaanza kuonyesha dalili za kuambukizwa

–Iwapo una dalili za kuugua

 • Iwapo utaanza kuonyesha au utapata dalili za COVID-19, hata ziwe ndogo, wafahamishe wasimamizi wako. Shirikiana nao kuchukua hatua zifaazo kusafiri kutoka hatua ya mwisho ya safari yako ya kuripoti hadi kwako nyumbani. Usichukue tu teksi ya kawaida
 • Fuata ushauri wa WHO, na CDC, au mamlaka za afya nchini humo kujikinga na kuwakinga wengine
 • Usiondoke kwako nyumbani kwa angalau siku 7 kuanzia siku dalili za kuugua zilipoanza kujidhihirisha (muda ambao utahitajika kutotoka kwako nyumbani ni tofauti kutoka nchi hadi nyingine, na hubadilika pia). Kufanya hivyo kutasaidia kutowaambukiza wengine
 • Jiandae mapema na uwaombe wengine usaidizi iwapo utahitaji. Mwombe mwajiri wako, na jamaa na marafiki wakusaidie kupata bidhaa unazozihitaji, na waziache nje ya mlango wako
 • Weka umbali salama ulioshauriwa kati yako na watu wengine nyumbani mwako ikiwezekana
 • Lala peke yako, ikiwezekana
 • Iwapo utalala pahala pamoja na wengine, nyote mnafaa kujitenga kipindi kilichoshauriwa. Mwongozo muhimu kuhusu hili unapatikana hapa. Tahadhari zaidi inafaa kuchukuliwa wakati wa kutumia bafu au chumba cha kuogea, choo na jikoni ili kuzuia kusambaza maambukizi
 • Osha mikono yako mara kwa mara kwa maji moto na sabuni kwa angalau sekunde 20
 • Kaa mbali na watu walio hatarini zaidi kutokana na maambukizi, kama vile wazee na wale walio na matatizo mengine ya kiafya kadiri iwezekanavyo
 • Huhitaji kuwapigia simu maafisa wa afya nchini mwako wakati wa kujitenga, ila tu iwapo dalili zitaanza kuwa mbaya wakati wa kipindi hicho cha kujitenga

Kifurushi cha Usalama cha CPJ kinawapa wanahabari na mashirika ya habari maelezo mengi ya msingi kuhusu usalama wa wanahabari kikiangazia mwili, akili na dijitali, na pia kinaangazia jinsi ya kuripoti kuhusu fujo za raia na uchaguzi.

[Angalizo la mhariri: Ushauri huu ulichapishwa mara ya kwanza mnamo Februari 10, 2020, na unafanyiwa mabadiliko mara kwa mara. Tarehe ya kuchapishwa inayoonyeshwa pale juu inaonyesha tarehe ya karibuni zaidi ya mabadiliko.]