Waandishi wa habari waliovalia vifaa kinga wakisubiri karibu na majengo ambapo wakazi wanawekwa karantini kwa sababu ya ugonjwa wa COVID-19 mjini Kiev, Ukraine, mnamo Aprili 28, 2020. (Reuters/Gleb Garanich)

Janga la COVID-19 likiendelea, mustakabali wa uhuru wa habari si mzuri. Hapa ni mambo kumi makuu

Na Katherine Jacobsen

Janga la ugonjwa wa COVID-19 limewapa kazi kubwa maafisa wa afya, limeathiri uchumi wa dunia, na kutumbukiza serikali kote duniani kwenye mzozo. Kadhalika, janga hili limeathiri jinsi wanahabari wanavyofanya kazi, miongoni mwa mengine kutokana na hali kwamba mamlaka katika mataifa mengi zimetumia ugonjwa huo kuminya uhuru wa vyombo vya habari.

Baadhi ya hatari zitafifia siku zinavyosonga: chanjo ya COVID-19 bila shaka itawakinga watu, wakiwemo waandishi wa habari, dhidi ya kueneza au kuambukizwa virusi hivi. Lakini baadhi ya hatua zilizowekwa zinazokandamiza uhuru wa wanahabari – ziwe za makusudi au zisizo za makusudi – huenda zikaendelea hata baadaye, wataalamu wanasema.

Kuna uwezekano kwamba hatua zilizochukuliwa kwa sababu ya virusi vya corona zitabadilisha kazi ya uanahabari kwa njia zisizoweza kutabirika, sawa na vile mashambulio ya Septemba 11, 2001, yalivyochochea sheria za kukabiliana na ugaidi kuenea duniani – na matokeo yake likasababisha ongezeko la visa vya wanahabari kufungwa, jambo linaloendelea hadi sasa..

Visa vya ukiukaji wa uhuru wa wanahabari duniani ambavyo CPJ imenakili kuhusiana na janga hili vinaweza kuwekwa kwenye makundi 10 ya kufuatiliwa kwa karibu (mifano imetolewa):

1. Sheria dhidi ya “taarifa za uzushi”

Janga hili limezipatia serikali kisingizio kipya cha kupitisha au kutekeleza sheria zinazoharamisha usambazaji wa “taarifa za uzushi,” “taarifa za kupotosha,” au “taarifa za uongo” – na kuzipa serikali sababu ya kutekeleza nyingine mpya. Katika kipindi cha miaka saba iliyopita, idadi ya wanahabari waliofungwa kwa makosa ya “taarifa za uzushi” au “taarifa za uongo” imeongezeka pakubwa, kwa mujibu wa utafiti wa CPJ..

Carlos Gaio, afisa wa kisheria wa ngazi ya juu nchini Uingereza anayefanya kazi na shirika la  Media Legal Defence Initiative, aliambia CPJ kwamba sheria za “taarifa za uzushi” zitaendelea kuenea serikali zikijaribu kudhibiti uenezaji wa habari kuhusu virusi hivi. Sheria hizo zitawaathiri wanahabari wa kawaida na wale wanaokabiliana na taarifa za uzushi bila kubagua. “Ni suala gumu kuharamisha kitu kama hicho [na ni] hatari sana,” Gaio alisema.

Taarifa za uzushi ni tatizo kubwa, lakini hatua hizi za kisheria zinazipa serikali uhuru wa kuamua ni habari gani zitaelezwa kuwa za uongo, jambo linalotoa ujumbe wa kuogofya kwa wanahabari wakosoaji wa serikali. Nchini Marekani, Rais Donald Trump mara kwa mara hukashifu ripoti za vyombo vya habari kuhusu COVID-19 na hutumia maneno ya kudhalilisha na kuwaita “taarifa za uzushi” anapotofautiana na ripoti hizo, mkakati ambao CPJ imebaini kwamba hufanikiwa katika kuvishusha hadhi vyombo ya habari na kupunguza imani ya umma kwenye vyombo hivyo. Desturi hii imekuwa kama ruhusa kwa watawala wa kiimla kuvidunisha na kuvihangaisha vyombo vya habari nchini mwao.

 • Afrika Kusini mnamo Machi 18 iliharamisha taarifa za uzushi kuhusu janga hili na adhabu yake ni pamoja na faini kubwa na kifungo jela – hatua ya kutia wasiwasi ikizingatiwa kwamba taifa hilo huwa kama mfano mwema kanda hiyo.
 • Puerto Rico, ambalo ni eneo la Marekani, mnamo Aprili 6 liliifanya kuwa hatia kwa vyombo vya habari “kueneza au kuruhusu kuenezwa” kwa “taarifa za uzushi”. Wanaokiuka sheria hiyo wanaweza kufungwa hadi miezi sita jela na kutozwa faini ya hadi $5000.

2. Kufungwa jela kwa wanahabari

Kukamatwa kwa wanahabari kumekuwa mbinu inayotumiwa na serikali za kiimla kwa kipindi kirefu kuzuia ripoti zinazokosoa serikali; takriban wanahabari 250 walikuwa jela kote duniani kwa mujibu wa hesabu ya mwisho ya CPJ ya kila mwaka iliyofanywa Desemba.  Wakati huu wa COVID-19, kufungwa jela kuna hatari kubwa; waandishi wanazuiliwa katika mazingira hatari kiafya na kulazimishwa kuwa karibu na watu wengine ambao wanaweza kuwa wameambukizwa. CPJ na mashirika mengine 190 kwa pamoja wametoa wito kwa watawala kote duniani kuwaachia huru wanahabari wote waliofungwa kwa sababu ya kutekeleza kazi yao.

Licha ya hayo, wanahabari bado wanakamatwa.

 • Nchini India, watawala katika jimbo la Tamil Nadu mnamo Aprili 23 walimkamata mwanzilishi wa tovuti ya habari ya SimpliCity na kumtuhumu kuwa alikuwa amevunja sheria ya zamani ya Magonjwa ya Mlipuko na sheria nyingine. Tovuti hiyo ilikuwa imechapisha ripoti zilizodai kulikuwepo na ufisadi serikalini wakati wa kusambaza chakula cha msaada kuhusiana na janga hili.
 • Jeshi nchini Jordan liliwakamata wanahabari wawili wa runinga ya Roya TV mnamo Aprili 10 kuhusiana na ripoti iliyoangazia malalamiko ya wafanyakazi kuhusu athari za kiuchumi za amri ya kutotoka nje.
 • Watawala nchini Somalia walimkamata mhariri wa shirika la habari la Goobjoog Media Group mnamo April 14 na kumtuhumu kwamba alieneza habari za uongo na kumvunjia heshima rais baada ya mwanahabari huyo kuchapisha ujumbe kwenye Facebook uliokosoa jinsi serikali ilivyokuwa inalishughulikia janga hili.

3. Kuzuia uhuru wa kujieleza

Baadhi ya hatua za dharura za serikali zimehusisha kubatilisha au kusimamisha haki ya uhusu wa kujieleza kipindi cha hali ya dharura.

 • Katiba ya Liberia hulinda uhuru wa kujieleza “ila tu wakati wa hali ya dharura” na humpa rais mamlaka ya “kuahirisha au kupunguza baadhi ya haki [na] uhuru” wakati wa hali ya dharura sawa na iliyoanza kutekelezwa Aprili 11.
 • Honduras mnamo Machi 16 ilitangaza hali ya dharura ya muda ambayo ilisimamisha utekelezaji wa baadhi ya vifungu vya katiba, kikiwemo kifungu kinacholinda haki ya uhuru wa kujieleza (ingawa serikali ilibadilisha hatua hiyo siku chache baadaye).

4. Udhibiti wazi wa habari, mtandaoni na nje ya mtandao

Mamlaka katika mataifa kadha zimesitisha uchapishaji na usambazaji wa magazeti katika kile ambacho walisema ni juhudi za kudhibiti kusambaza kwa COVID-19. Kwingineko, mamlaka zinazosimamia vyombo vya habari zimefungia mitandao ya habari au kuondoa makala za mtandaoni zinazokosoa serikalil.

 • Jordan, Oman, Morocco, Yemen, na Iran zote zilisimamisha usambazaji wa magazeti Machi.
 • Tajikistan iliifungia tovuti huru ya habari ya Akhbor Aprili 9, baada ya kuchapishwa kwa taarifa zilizoikosoa serikali.
 • Mamlaka inayosimamia vyombo vya habari Urusi kwa jina Roskomnadzor, iliamuru kituo cha redio cha Ekho Moskvy kutopeperusha mahojiano na mtaalamu wa magonjwa, na mtandao wa habari wa Govorit Magadan ulishurutishwa kuondoa mtandaoni makala kuhusu kifo kilichotokana na nimonia.

5. Kuwatishia na kuwashambulia wanahabari, mtandaoni na nje ya mtandao

Maafisa wa serikali na raia wa kawaida wamejibu ripoti za uokosoaji kuhusu hatua waliochukua kukabiliana na janga hili kwa hasira na vitisho. Katika maeneo ambapo mazingira ya uanahabari tayari yalikuwa hatari, hali imekuwa hatari zaidi.

 • Kiongozi wa Chechnya, Ramzan Kadyrov, alimtishia mwandishi wa Novaya Gazeta baada yake kuandika mnamo Aprili 12 kwamba Wachechen walikuwa wameacha kupiga ripoti wanapokuwa na dalili za virusi vya corona kwa hofu ya kubandikwa kuwa “magaidi”.
 • Wanahabari nchini Haiti walishambuliwa na wanaume wasiojulikana katika Afisi ya Taifa ya Vitambulisho mnamo Aprili 2 waliokuwa wanachunguza madai kwamba afisi hiyo ilikuwa inakiuka mwongozo wa COVID-19 wa watu kukaa mbali na wengine.
 • Wanajeshi wa Ghana waliokuwa wakitekeleza masharti kuhusiana na janga hili waliwapiga wanahabari wawili katika visa viwili tofauti Aprili.

6. Mahitaji ya kupata kibali na kupunguzwa kwa uhuru wa kusafiri

Mamlaka zimepunguza uwezo wa wanahabari kusafiri na kutembea kwa njia huru, kwa mfano wanapotaka kuripoti wakati wa amri ya kutotoka nje, au kuingia hospitalini kupata taarifa za moja kwa moja kuhusu huduma hospitalini. Wakati mwingine wanahabari wanapewa vibali maalum, lakini kuwahitaji wanahabari kuwa na vitambulisho vinavyotolewa na serikali kunawaruhusu viongozi kuamua ni nani ataruhusiwa kuhudumu kama mwanahabari.

Utafiti wa unaonyesha kwamba hii inaacha wazi uwezekano wa kuwazuia wale wasiofanyia kazi mashirika makubwa ya habari au wale wanaokosoa watawala.

 • Polisi nchini India waliwashambulia wanahabari wanne katika visa vitatu tofauti Hyderabad na Delhi mnamo Machi 23 walipokuwa wanasafiri kwenda au kutoka kazini wakati wa zuio la kutosafiri, hata ingawa serikali ya kitaifa imeeleza kwamba wanahabari hawaathiriwi na zuio hilo la kutosafiri.
 • Nigeria nayo iliwahitaji wanahabari kuwa na kitambulisho kuwawezesha kusafiri katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa na zuio la usafiri, ikiwemo mji mkuu Abuja, na ilitangaza kwamba ni wanahabari 16 pekee walioruhusiwa kuingia makao ya rais.

7. Kuzuia kufikiwa kwa habari

Sheria kuhusu uhuru wa kupata habari zinazoruhusu wanahabari kuitisha data, taarifa na stakabadhi za serikali zimesimamishwa. Mikutano na hafla ya kiserikali ambazo wanahabari huhudhuria zimehamishiwa mtandaoni, ambapo kuna viwango mbalimbali vya kuruhusiwa kwa wanahabari kushuhudia au kupata habari. Nchini Marekani, uhasama wa Trump dhidi ya wanahabari unatoa mfano mbaya kwa maafisa wa serikali za majimbo na mitaa.

Gaio aliambia CPJ kwamba mitindo hii huenda ikaendelea. “[Serikali] zitaifanya kuwa vigumu kwa maafisa kutoa habari. Kufikiwa kwa habari kutachukua muda, na itakuwa pia vigumu kwa wanahabari kufika au kufikia maeneo ya umma kutokana na hatari ya kuambukizwa,” alisema.

 • Rais wa Brazil Jair Bolsonaro mnamo Machi 23 aliidhinisha hatua ya kisheria inayosimamisha makataa yanayokuwepo kwa maafisa wa umma na taasisi kujibu maombi ya habari, na pia hatua hiyo inaondoa fursa ya kukata rufaa iwapo ombi litakataliwa. (Mahakama ya Juu ya Brazil ilibatilisha hatua hiyo mnamo Aprili 30, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari.)
 • Magavana na mameya Marekani wameweka pia masharti mbalimbali ya kufikia vikao na wanahabari kote nchini humo. Gavana wa jimbo la Florida, mnamo Machi 28, alimzuia mwanahabari mmoja kuhudhuria kikao cha wanahabari alipouliza swali kuhusu hitaji la watu kutokaribiana.

8. Kufurushwa na kunyimwa viza

Ili kudhibiti taarifa kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali kuhusu COVID-19, baadhi ya mataifa yameanza kutowavumilia wanahabari wa mashirika ya nje, ambao katika baadhi ya mataifa kwa kawaida wamekuwa na uhuru wa kuripoti taarifa zinazokosoa serikali kuliko wanahabari wa mashirika wenyenji.

 • China na Marekani zimekuwa kwenye hali ya vuta nikuvute kuhusu uhuru wa wanahabari tangu mapema 2020. Miongoni mwa yaliyotokea: Februari, China iliwafurusha wanahabari watatu wa Wall Street Journal, katika kilichoonekana kama kulipiza kisasi kuhusu kichwa cha habari kwenye makala ya maoni kuhusu COVID-19. Machi, Marekani nayo iliweka kikomo cha wanahabari wa vyombo vya serikali ya China ambao wangepewa viza kuwa 100; China nayo ilijibu kwa kufutilia mbali viza za  wanahabari 13 wa Marekani kutoka The New York Times, The Washington Post na The Wall Street Journal.
 • Misri ilimfukuza mwandishi wa habari wa Guardian Ruth Michaelson kulipiza kisasi taarifa yake ya Machi 15 iliyotilia shaka takwimu zilizokuwa zikitolewa na serikali kuhusu janga hilo.

9. Upelelezi na kuwafuatilia watu

Serikali katika nchi mbalimbali duniani zinafuatilia data za simu kuhusu walipo na wanakoenda watu na pia zinafanyia majaribio au kuanza kutumia program tumishi mpya za kuwafuatilia watu za kutumiwa kufuatilia usambaaji wa COVID-19, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari. Upelelezi na ufuatiliaji huu unaweza kuwa tishio kwa usiri wa wanaotoa habari kwa wanahabari. Mifumo inaanza kutekelezwa bila uangalizi na usimamizi wa kutosha, na huenda ikaendelea kutumika muda mrefu baada ya janga hili kumalizika.

 “Kumekuwepo na wasiwasi kwamba hali za dharura hutengeneza vipimo vipya vya matarajio ya viwango vya ufuatiliaji wa watu ambavyo serikali zinaruhusiwa kuufanya. Bila shaka tulishuhudia hili likitokea baada ya 9-11, lakini nafikiri suala hilo linajitokeza sasa pia,” anasema  Carrie DeCell, mwanasheria katika taasisi ya kutetea uhuru wa kujieleza Knight First Amendment Institute jijini New York. “Vitendo ambavyo vinaweza kukubalika katika hali kama hiyo havifai kukubalika baada ya serikali kudhibiti janga hili na baada ya janga hili kufifia siku zijazo.”

David Maass, mtafiti mchunguzi wa ngazi ya juu katika wakfu wa Electronic Frontier Foundation wenye makao yake San Francisco, anakubali kwamba kila vyombo vya utekelezaji wa sheria vinapokabidhiwa teknolojia mpya, huwa vigumu kuvipokonya. “Tumeona kwamba sasa wanaitumia kwa sababu ya kukabiliana na virusi hivi hatari,  lakini hatujui kitakachotokea baadaye.”

 • Kampuni za mawasiliano ya simu Italia, Ujerumani, na Austria zimekuwa zikikabidhi data kuhusu mienendo ya watu kwa maafisa wa afya ya umma, ingawa zimechanganywa na majina kufichwa; serikali za Korea Kusini na Afrika Kusini zinafuatilia mwenendo wa simu binafsi, na Israel majuzi iliwapa idhini maafisa wa usalama kupata data kuhusu mwenendo wa mtu na data nyingine kutoka kwa mamilioni ya watu wanaotumia simu za mkononi.

10. Hatua za Hali ya Dharura

Watawala wa kiimla wanaweza kuchukua nafasi kujifaidi wenyewe kupitia hatua za hali ya dharura ambazo zinaharamisha au kuweka masharti ya watu kukusanyika, kama ambavyo CPJ imenakili awali. 

 • Bunge nchini Hungary mnamo Machi 30 liliidhinisha sheria kadha za hali ya dharura zinazomwezesha Waziri Mkuu Viktor Orbán kutawala kwa amri yake mwenyewe.
 • Thailand mnamo Machi 26 ilianza kutekeleza hali ya dharura inayoiruhusu serikali “kusahihisha” ripoti au taarifa ambazo inaamini si sahihi na inaruhusu wanahabari kufunguliwa mashtaka chini ya Sheria ya Uhalifu wa Kompyuta, ambayo adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano jela.

Huku mataifa mengi yakiwa bado yako chini ya hali ya dharura inayowapa watawala nguvu nyingi za kutawala kwa amri – na virusi hivi ikiwa ndio tu vinaanza kuathiri zaidi mataifa yanayoendelea – kuna uwezekano masharti na vizingiti zaidi vikawa njiani.